
Sifa za Kujiunga Shule za Kidato Cha Tano Tanzania
Baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutangaza matokeo ya Kidato cha Nne, fikra za wahitimu pamoja na walezi wengi huelekezwa kwenye jambo moja muhimu ikiwa mwanafunzi atachaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule za serikali.
Kwa wengi, ndoto ya kuendelea na masomo katika ngazi ya juu kupitia shule bora za umma inaendelea kuwa kipaumbele kutokana na ubora wa elimu unaotolewa pamoja na gharama nafuu ya ada ukilinganisha na shule binafsi.
Hata hivyo, mchakato wa kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano si rahisi. Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeweka vigezo mahsusi vinavyopaswa kuzingatiwa na wanafunzi wote wanaotamani kujiunga na shule hizi.
Kwa mwaka 2025, vigezo hivi vitatumika kama msingi wa kuchagua wanafunzi watakaodahiliwa kwenye shule za serikali pamoja na shule binafsi.
1. Ufaulu wa Masomo Muhimu
Mwanafunzi anatakiwa kuwa amefaulu masomo yasiyohusiana na dini kwa kiwango cha alama A, B au C katika angalau masomo matatu. Hili ni kigezo cha msingi kinachoonyesha utayari wa mwanafunzi kuendelea na masomo ya juu. Masomo ya dini hayaingii katika hesabu hii, hivyo wahitimu wanapaswa kuhakikisha kuwa masomo yao ya msingi ya kitaaluma yamepata alama za kuridhisha.
2. Jumla ya Alama (Pointi 7 Bora)
Kwa mujibu wa muongozo wa udahili, jumla ya alama katika masomo saba bora haipaswi kuzidi alama 25. Kigezo hiki kinasaidia kuchuja wanafunzi walioonyesha uwezo wa kitaaluma wa juu katika muktadha mpana wa masomo. Hivyo, mwanafunzi anatakiwa kuzingatia ufaulu mzuri katika masomo yote ya msingi.
3. Alama za Masomo ya Tahasusi
Mwanafunzi anatakiwa kuwa na jumla ya alama kati ya 3 hadi 10 katika masomo ya tahasusi — yaani yale anayotarajia kuyaendeleza katika Kidato cha Tano. Aidha, mwanafunzi hatakiwi kuwa na alama ya “F” katika somo lolote kati ya haya. Kukosa ufaulu katika mojawapo ya masomo ya tahasusi kunaweza kumwondoa kwenye orodha ya waliochaguliwa.
4. Kikomo cha Umri
Kigezo kingine kinachozingatiwa ni umri wa mwanafunzi. Kwa mwaka 2025, mwanafunzi anayetuma maombi ya kujiunga na Kidato cha Tano anapaswa kuwa na umri usiozidi miaka 25. Lengo la kigezo hiki ni kuhakikisha kuwa wahitimu wanadumu kwenye mfumo wa elimu kwa wakati unaostahiki.
5. Ushindani wa Nafasi Shuleni
Hata kama mwanafunzi amekidhi vigezo vyote hapo juu, bado kuchaguliwa kwake kunategemea ushindani wa nafasi zilizopo katika shule husika. Hii ina maana kuwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi katika kundi la waombaji ndiyo watakaopata nafasi kwa kipaumbele. Ushindani huu huzingatiwa kulingana na masharti ya usajili wa shule na vipaumbele vya tahasusi.
Kwa Shule Binafsi: Nafasi Zipo kwa Walio na Ufaulu Tofauti
Tofauti na shule za serikali, shule binafsi zinaweza kutoa fursa kwa wanafunzi waliokosa vigezo vya udahili wa serikali lakini bado wana sifa za kitaaluma. Mwanafunzi anatakiwa:
- Awe na angalau alama A, B au C kwenye masomo matatu yoyote katika mtihani wa Kidato cha Nne;
- Awe na division ya I hadi III;
- Asiwe na alama “F” kwenye masomo ya mchepuo; AU
- Hata bila kujali division, awe na alama C tatu katika masomo ya mchepuo.
Hitimisho
Kwa wale wanaotaka kusoma kama Private Candidate (PC) kwa ajili ya Mtihani wa Kidato cha Sita, wanatakiwa:Kuwepo na historia ya kufanya mtihani wa Kidato cha Sita (Resitter wa ACSEE);
Kuwa na alama A, B au C tatu katika masomo yoyote, si lazima ya mchepuo.